Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amezitaka Tanzania na Rwanda kuongeza kasi katika mipango ya kuanzisha miradi ya pamoja ya miundombinu, ukiwamo ujenzi wa reli mpya kuunganisha nchi hizo mbili.
Rais Kikwete ametoa wito huo wakati alipozungumza na Balozi mpya wa Rwanda katika Tanzania, Mheshimiwa Benjamin Ruganguzi, baada ya balozi huyo kuwasilisha kwa Rais Kikwete hati zake za utambulisho katika halfa fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es salaam, leo, Jumanne, Mei 22, 2012.
Baada ya kuwa amemkaribisha Tanzania kwa kumhakikishia kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda ni mzuri na unaendelea kuwa wa karibu zaidi, Rais Kikwete amemwambia Balozi Ruganguzi, “Kazi kubwa na ya kwanza Mheshimiwa Balozi iwe ni kusaidia kuhakikisha kuwa mradi wa ujenzi wa reli unaanza mapema iwezekanavyo.”
Tanzania na Rwanda zimekubaliana kujenga reli kati ya Isaka, Tanzania hadi Kigali, Rwanda, reli ambayo itaunganisha pia nchi jirani ya Burundi. Nchi hizo mbili zinafanya jitihada za pamoja kuwasiliana na kuzungumza na wafadhili na makampuni binafsi ya kimataifa kuangalia uwezekano wa kupatikana kwa uwezeshwaji wa kujengwa kwa reli hiyo.
Katika mazungumzo yao, Rais Kikwete na Balozi Ruganguzi pia wamekubaliana kuanza ujenzi ama kukarabati miundombinu nyingine inayotakiwa kuanzishwa ama inayotumiwa kwa pamoja na nchi hizo ukiwamo ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwenye Mto Rusumo, kupanua daraja linalounganisha nchi hizo kwenye mto huo na pia kukarabati Reli ya Kati inayosafirisha mizigo ya Rwanda.
Ili kuhakikisha kuwa anakuwa na ufutiliaji wa karibu juu ya miradi hiyo, Rais Kikwete amemshauri Balozi Ruganguzi kuhakikisha kuwa anatembelea bila kuchoka Wizara ya Uchukuzi pamoja na taasisi zake kama vile Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Bandari ya Dar es Salaam.
“Ushauri wangu kwako ni kwamba jipe muda wa kuwatembelea mara kwa mara maofisa wa Wizara ya Uchukuzi na taasisi zake kama vile TRC na Bandari ili uweze kupata habari za uhakika kuhusu miradi yetu ya pamoja,” Rais amemwambia Balozi Ruganguzi.
Rais pia amemhakikishia balozi huyo kuwa Tanzania itaendelea kuhudumia mizigo ya Rwanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam na kutumia Reli ya Kati na barabara za Tanzania.
No comments:
Post a Comment