Sunday, May 6, 2012

MAMA KIKWETE AWATAKA WANASACCOS KULIPA MADENI KWA WAKATI


Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wanachama wa Chama cha kuweka Akiba na Kukopa cha URSINO na REGENT (URESCO) kuwa na utaratibu maalum wa kukusanya madeni ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote watakaochelewa kulipa madeni yao.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliyasema hayo jana wakati akifungua SACCOS hiyo iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliendelea kusema kuwa ili SACCOS iweze kuendelea ni lazima ijiwekee utaratibu wa kutoa  mafunzo na semina mbalimbali za kuwajengea uwezo wanachama wake  katika uendeshaji na kusimamia miradi ya jamii.
“SACCOS hii itakuwa imetoa mchango mkubwa kwa jamii ikiwa itaweza kuwasaidia vijana na wakinamama kutumia mitaji waliyoipata kwa kuanzisha na kuendelea miradi ya kuongeza kipato na hatimaye kipato hicho kikawasaidia wazee wastaafu ambao pia wanahitaji msaada kutoka kwa vijana na kina mama hao”, alisema Mama Kikwete.
Mama Kikwete pia  aliitaka SACCOS hiyo kujiwekea  dhamira ya kupata maendeleo makubwa zaidi kwa kuendelea kuweka akiba na kuwa makini katika kurudisha mikopo ili kuweza kuwavutia wanachama wengi zaidi kujiunga kwani mafanikio yao yatatokana na kuwa na idadi kubwa ya wanachama ambao wana akiba ya kutosha.
Akisoma taarifa ya SACCOS hiyo Jonathan Kasesela ambaye ni Mwanachama alisema kuwa Chama hicho chenye wanachama 242 wenye hisa zaidi ya shilingi milioni 18 na amana zaidi ya shilingi milioni 128 ilianzishwa mwaka 2006.
“Malengo tuliyonayo ni kuongeza idadi ya wanachama, kujenga ofisi ya kudumu, kuwasaidia wazee wastaafu katika eneo la Ursino na Regent ambao ni asilimia 80 ya wakazi wote wa eneo hili wapatao 1800, kusaidia vikundi vya vijana  na wanawake katika juhudi za maendeleo”, alisema Kasesela.
 
Mwezi Julai mwaka 2007 chama hicho kilianza kukopesha wanachama hadi kufikia sasa wanachama waliopata mkopo ni 219 ambao wamekopa zaidi ya shilingi milioni 136.
Taasisi ya WAMA iliichangia SACCOS hiyo shilingi milioni tatu fedha ambazo zitatumika kuongeza mtaji wa mfuko wa umoja huo.Chanzo:fullshangweblog

No comments:

Post a Comment