Wednesday, May 23, 2012

Hakuna atakayepora ardhi ya wananchi – Rais Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mipango mikubwa ya kuendeleza kilimo inayopangwa ama tayari inaendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi hailengi kupora adhi ya wananchi na badala yake inalenga kuongeza thamani kwenye ardhi hiyo kwa manufaa ya pande zote zinazojihusisha na kilimo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa siyo wawezekezaji wote wanaotaka kuingia katika sekta ya kilimo wataokuwa wanaendesha shughuli ya moja kwa moja ya kilimo bali watawekeza katika huduma na raslimili za kuhudumia na kuunga mkono maendeleo ya kilimo.
Rais Kikwete ameyasema hayo, Jumanne, Mei 22, 2012, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Biashara wa Marekani, Mheshimiwa Michael Camunez ambaye yuko katika ziara ya Tanzania tokea Jumamosi iliyopita.
Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na kwamba Serikali inafanya jitihada kubwa za kuendeleza kilimo, pengine kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya Tanzania huru, bado ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa inaendelea kulinda ardhi ya wakulima wadogo na kuwawezesha kunufaika na uwekezaji wa sekta binafsi ndani ya ardhi yao wenyewe.
Rais Kikwete amesema pia kuwa ni vigumu kwa wawekezaji wa sekta binafsi kupora ardhi ya wananchi katika Tanzania kwa sababu kila wilaya katika Tanzania ina benki ya ardhi ambayo ndiyo itatolewa kwa wawekezaji wa sekta binafsi na wala siyo ardhi ya wananchi.
“Sekta binafsi inakuja kuwekezaji katika kilimo na wala siyo kupora ardhi ya wananchi. Wale wawekezaji wa sekta binafsi watapewa ardhi kutoka kwenye benki za ardhi za wilaya mbali mbali na hakuna atakayegusa ardhi ya wananchi,” amesema Rais Kikwete katika mazungumzo na Naibu Waziri huyo ambaye nchi yake ya Marekani ni moja ya nchi ambayo makampuni yake yanataka kuingia katika maendeleo ya kilimo katika Tanzania.
Kuhusu sekta binafsi kuwekeza katika kilimo, Rais Kikwete amesema kuwa siyo kila mwekezaji atakuja kulima. “Wengine watakuja kuwekeza katika kuzalisha mbegu bora zaidi, wengine kama kampuni ya Yara watakuja kuwekeza katika uzalishaji na usambazaji wa mbolea, wengine watakuja kuingia katika uzalishaji na usambazaji wa mashine za kilimo, wengine katika uzalishaji wa madawa ya kilimo na wengine katika kutoa huduma za kifedha kwa wakulima,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Wengine wanaweza hata kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao ya wakulima na ya kilimo.”

No comments:

Post a Comment