Imeelezwa kuwa Simba ilisafiri kwa masaa manne kwa njia ya barabara kutoka Khartoum hadi Shendi jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za CAF zinazozungumzia umbali usiozidi masaa mawili, kwani kanuni ya CAF kifungu cha 5 (3) kinazungumzia umbali wa kusafiri kwa basi usizidi kilomita 200. Aidha, kwa upande wa malazi, kanuni ya CAF kifungu cha 7 (c), inaeleza kuwa timu mwenyeji inatakiwa kuhakikisha kuwa timu mgeni inaishi katika hoteli ya daraja la kwanza na pia msafara mzima unakaa katika hoteli moja, lakini Simba iliwekwa katika hosteli inayofanana na mabweni ya wanafunzi na imepewa vitanda 24 tu huku msafara ukiwa na watu takribani 30. Kama hiyo haitoshi, ukosefu huo wa vyumba uliwalazimu viongozi wa Simba wakiwemo Mwenyekiti wake Ismail Aden Rage kulala kwenye makochi ya chumba cha mapokezi pamoja na kocha msaidizi wa makipa wa Simba, James Stephan Kisaka, huku mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Swedy Mkwabi na kiongozi wa msafara, Hussein Mwamba ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF walilazimika kwenda kulala nje ya hosteli hiyo ya Shendi. Kwa mujibu wa ofisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga ambaye ameambatana na Simba Sudan, pamoja na hujuma hizo bado kikosi chake kina ari kubwa ya mchezo huo huku wachezaji wakiahidi kufanya mambo makubwa katika mchezo huo. Kamwaga alisema hujuma hizo zimewapa changamoto zaidi ya kujipanga kuhakikisha wanashinda kufa kupona ili kushinda na kusonga mbele kwenye michuano hiyo. “Tunashukuru mungu pamoja na hila za hapa na pale tulizofanyiwa tangu tufike huku hatujavunjika moyo, wachezaji wameshajengwa kisaikolojia hivyo wanasubiri kutimiza wajibu wao tu,”alisema Kamwaga.
Alisema wachezaji wa Simba chini ya kocha wake Mkuu Mserbia Milovan Cirkovic ilifanya jana ilifanya mazoezi yake ya mwisho kabla ya mchezo huo, ambapo kocha huyo ameahidi kuendeleza ubabe kwa Wasudan hao. Simba imekwenda Sudan ikiwa na furaha ya ubingwa wa ligi kuu bara sambamba na kuwafunga mabao 5-0 mahasimu wao Yanga katika mchezo wa mwisho, imepania kushinda mchezo huo ili kutotibua furaha zao. Ili Simba iweze kusonga mbele inahitaji sare yoyote au kufungwa chini ya mabao 3-0, ambapo ushindi utaifanya ikutane na timu zilizotolewa hatua ya 16 bora ya ligi ya mabingwa katika mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi.Chanzo:http://mamapipiro.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment