Thursday, June 7, 2012

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dk Terezya Huvisa Akutana na Kamati ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Mazingira


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dk Terezya Huvisa akizungumza na Kamati ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Mazingira kwenye ukumbi wa Hazina kulia Mwenyekiti wa Kamati hiuo James Lembeli kushoto Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Charles Kitwanga,Naibu katibu Mkuu Eng Ngosi Mwihava,Mh Zakhia Megji kikao hicho kimefanyika leo Mjini Dar es Salaam.Picha na Ali Meja

MILIONI 421.8 ZAPATIKANA KUCHANGIA MPANGO WA ELIMU KATA YA KIPAWA JIJINI DAR ES SALAAM

Mgeni rasmi wa harambee hiyo akimpa mkono wa asante mwakilishi wa kampuni ya Home Shopping Centre Bi Madiha Al Harthy (kushoto),Salma baada ya kuchangia sh. milioni 22...

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Dk. Makongoro Mahanga (kulia), Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa (kushoto) na Mwenyeji wa harambee ya kuchangia mpango wa elimu wa Kata ya Kipawa, Diwani wa Kata  hiyo Bonah Kaluwa, wakimuongoza Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye alikuwa mgeni rasmi kuingia ukumbini Katika hafla iliyofanyika jana usiku ndani ya hoteli ya Kilimanjaro (Kempiski hotel) jijini Dar es Salaam . 
(PICHA NA PHILEMON SOLOMON WA FULLSHANGWE)
Wadau mbalimbali wakiwa kwenye harambee hiyo
Diwani wa Kata ya Kipawa Bonah Kaluwa, akitoa neno la shukurani kabla ya kuanza kwa harambee hiyo...
Mkurugenzi wa SONGAS Limited Bw;Christopher Ford(katikati),akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya dolla za kimarekani 10,000, mgeni rasmi wa harambee hiyo.kushoto meneja 
rasilimali Songas Bi Agatha Keenja...
 
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja (katikati) akipongezwa na Mgeni rasmi wa harambe hiyo baada ya kuchangia sh. 500,000...
 

eya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa (kushoto), akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya sh.milioni 10, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyekuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia mpango wa elimu Kata ya Kipawa, iliyofanyika Dar es Salaam juzi. Fedha hizo zilitolewa na Manispaa hiyo ambapo zaidi ya sh. milioni 400 zilipatikana.
Na Dotto Mwaibale

Wednesday, June 6, 2012

Dawa Za Kulevya Zaitikisa Iringa



Na Mwandishi Wetu

BIASHARA ya dawa za kulevya imeshika kasi mkoani Iringa huku vigogo kadhaa wakitajwa kuhusika, Kwanza Jamii-Iringa linaripoti.
Taarifa zinaeleza kwamba, wafanyabiashara kadhaa maarufu mkoani humo wanatajwa kujihusisha katika usambazaji na utumiaji wa dawa hizo, hususan cocaine, heroin na Mandrax.
Kundi rika la vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 35 ndilo linaloongoza kwa biashara hiyo kwa utumiaji na usambazaji, huku bhangi ikiwa inaongoza miongoni mwa orodha ya dawa za kulevya.
“Huwezi kuipiga vita biashara ya dawa za kulevya ikiwa vigogo wenyewe ndio wanaosambaza na kutumia. Wapo wanajulikana, lakini hatujui ni kwa vipi serikali inashindwa kuwakamata,” kimeeleza chanzo chetu cha habari.
Inaelezwa kuwa, wafanyabiashara kadhaa wa mjini humo, ambao baadhi wanadaiwa kuwemo kwenye orodha ya vigogo 58 wa dawa za kulevya iliyopelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2006, ndio miungu-watu wanaojificha kwenye mwavuli wa biashara zao halali pamoja na kusaidia jamii.
Taarifa zinaeleza kwamba, vigogo wengi na hasa wenye fedha, ndio watumiaji wakubwa wa dawa za viwandani kama heroin na cocaine kwa vile hawawezi kwenda kununua bhangi mitaani kutokana na hadhi zao, huku kundi kubwa la vijana likitajwa kutumia zaidi bhangi.
Wananchi kadhaa waliohojiwa na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema matumizi ya dawa za kulevya mkoani humo yanazidi kushika kasi licha ya serikali kusema yamepungua.
“Huku mitaani sisi ndio tunaowaona watumiaji, wanaongezeka kila wakati na hakuna juhudi za kuwapunguza, hasa vijana ambao wanazidi kuathirika na matumizi hayo,” walisema wananchi hao.
Kauli hiyo ya kukithiri kwa matumizi ya dawa za kulevya iliungwa mkono na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kitanzini iliyo katikati ya Manispaa ya Iringa, Raphael Magata, ambaye alisema matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana yanazidi kuongezeka.
Magata alisema kwamba, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali pamoja na asasi mbalimbali za kijamii kuelimisha juu ya madhara yake, lakini idadi ya vijana wanaojihusisha na biashara hiyo inazidi kuongezeka, hivyo kuitaka jamii ishiriki kupambana ili kuokoa nguvu kazi isipotee.
“Vijana wengi hivi sasa wanajihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya ingawa serikali inajitahidi kuwalimisha madhara yake kwa kushirikiana na asasi binafsi. Madhara yake ni makubwa kwa sababu yanachangia pia maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi,” alisema Magata.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba, alisema kwamba, jeshi lake linajitahidi kupambana na matumizi na biashara ya dawa hizo za kulevya, kwa kushirikiana na jamii kupitia Ulinzi Shirikishi.
Soma zaidi ...http://www.kwanzajamii.com

Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wala Kiapo

Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) leo wameapishwa rasmi kushika madaraka hayo huku Tanzania ikiwa na Wawakilishi tisa katika Bunge hulo.

Wabunge hao waliapa baada ya kupatikana Spika wa mpya wa Bunge hilo ambapo safari hii ikiwa ni Uganda kushika Uongozi huo wa Juu wa Bunge na Mwana Uchumi, Margareth Zziwa kuchukua nafasi hiyo.

Wabunge wote wa Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya Mashariki waliokula kiapo hii leo ni pamoja na Mwenyekiti wa Wabunge wa Tanzania kwenye Bunge EALA, Alhaj Adam Omar Kimbisa na Katibu wake, Mh Shy-Rose SaddrudinBhanji.

Wengine ni Mhe. Anjela Charless Kizigha, Mh. Maryam Ussi Yahya,Mh.Nderkindo Perpetua Kessy, Dkt Twaha Issa Taslima, Mhe. Abdullah Ali Hassan Mwinyi, Mhe Bernard Musomi Murunyana Mhe. Charles Makongoro Nyerere na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta anaeingia kwa wadhifa wake wa Uwaziri.

Wabunge hao wameapisha pamoja na wabunge wenzao wa Kenya, Uganda, Rwanda na katika picha juu ni Waziri wa Afrika Mashariki na mbunge wa Urambo Mh Samwel Sitta akiapa katika bunge hilo jana jijini ArushaSOURCE: FATHER KIDEVU BLOG

MBUNGE WA SEGEREA AWATAKA WADAU WA ELIMU KUJITOKEZA KATIKA HARAMBEE YA KATA YA KIPAWA KATIKA HOTELI YA HYATT KILIMANJARO

Diwani wa Kata ya Kipawa Manispaa ya Ilala Dar es Salaam, Bonah Kaluwa (kushoto), akiwa katika moja ya mikutano ya maendeleo kwenye kata yake. Kulia ni Katibu  wa Kata hiyo Amina Sabo na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Karakata, Greyson Malick. (PICHA NA DOTTO MWAIBALE)
 
 
Na Dotto Mwaibale

MBUNGE wa Jimbo la Segerea Dk. Makongoro Mahanga amewataka wadau wa elimu kujitokeza leo kuchangia mfuko wa elimu wa Kata ya Kipawa katika harambee itayoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempiski.

Alisema Kata ya Kipawa ni moja ya kata iliyopo katika jimbo la Segerea na Manispaa ya Ilala zenye upungufu mkubwa wa miundombinu na vifaa katika shule zake za msingi na za sekondari za serikali.

Alisema upungufu huo ni pamoja na uchache wa shule, upungufu wa madarasa, madawati, matundu ya vyoo, ofisi za walimu, meza na viti vya walimu, maabara na nyumba za walimu.
" Upungufu huu wa mahitaji katika shule za kata ya Kipawa, ni tatizo la mkoa mzima wa Dar es Salaam, na wilaya nzima ya Ilala hivyo ni wajibu wetu kusaidia". alisema Mahanga

Alisema katika suala la elimu serikali ya awamu ya nne imefanya mengi mazuri ingawa bado kuna changamoto kadhaa ambapo kwa mkoa wa Dar es Salaam,  kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaosoma shule za awali, shule za msingi na shule za sekondari.

Aliongeza kuwa kwa sasa kuna wanafunzi 26,121 wa shule za awali katika mkoa wa Dar es Salaam, kati yao wanafunzi 7,499 wako katika wilaya ya Ilala. Mkoa wa Dar es Salaam pia kwa sasa una wanafunzi 510,269 wanaosoma shule za msingi, kati yao wanafunzi 152,135 ni wa wilaya ya Ilala.

Alisema  kuna wanafunzi 204,684 wa shule za sekondari katika mkoa wa Dar es Salaam, kati yao wanafunzi 57,890 wako katika wilaya ya Ilala. Katika mkoa wa Dar es Salaam, kuna shule 315 za sekondari, kati yake shule 135 ni za serikali.

" Nguvu za wananchi zimetumika sana hasa katika ujenzi wa shule za sekondari nchini na kuungwa na serikali ambapo kwa mkoa   wa Dar es Salaam kati ya shule hizo za serikali 135, shule 124 ni za wananchi zilizojengwa kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na Halmashauri za wilaya." alisema Mahanga.

Alisema shule hizo 124 za wananchi za mkoa wa Dar es Salaam, wilaya ya Ilala ina shule 40 za sekondari za wananchi, ambazo karibu zote zimejengwa kuanzia mwaka 2006.

Alisema Shule hizo nyingi zinachangamoto na upungufu wa vyumba vya madarasa 5,526, kati yake wilaya ya Ilala ina upungufu wa madarasa 1,459, ofisi za walimu 466,nyumba za walimu 14,788.

Alisema katika mkoa wa Dar es Salaam kuna upungufu wa madawati 58,764 kwa shule za msingi na 45,349 kwa shule za sekondari. Kati ya hizo wilaya  ya Ilala ina upungufu wa madawati 18,030 kwa shule za msingi na madawati 19,534 kwa shule za sekondari.
Alisema matundu ya vyoo 18,558 yanahitajika kwa mkoa wa Dar es Salaam, huku wilaya yenu hii ya Ilala ikihitaji matundu ya vyoo 4,886.

Alisema katika uchangia wa elimu hatuwezi kuiachia serikali pekee, kwani uwezo wa serikali yetu ni ndogo hivyo alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa kata ya Kipawa wakiongozwa na diwani wao, Bonnah Kaluwa kwa kubuni mradi wa uchangiaji miundombinu ya shule katika kata hiyo.

Tuesday, June 5, 2012

BATA ZA DOGO RAMA WA TWANGA PEPETA...

 

Nyota wa Muziki wa Dansi Dogo Rama(kushoto) aki- shoo luv kiaina na mshikaji wake ndani ya viwanja vya Leaders Club , Kinondoni jijini dar es salaam Jumapili wiki iliyopita.

CCM Wametua Njombe Leo..

 








Picha zote: Bashir Nkoromo

Ali Suleiman "Aurora" afariki dunia na kuzikwa Kisutu

 

MDAU wa michezo na burudani hapa nchini, Ally Suleiman 'Aurora' amefariki usiku wa kuamkia jana na kuzikwa kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana ilieleza kwamba Aurora alifikwa na mauti baada ya kuugua kwa muda mrefu na kulazwa kwenye hospital ya Muhimbili.
Enzi za uhai wake Aurora aliweza kufadhili mashindano ya urembo, sambamba na michezo mbalimbali ikiwamo ngumi.
Miongoni mwa mabondia waliofanikiwa kwa msaada wa Aurora ni bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Awadh Tamim ambaye alisaidiwa na Aurora kutimiza ndoto hizo.
Mbali na Tamim, Aurora aliweza kuisadia timu ya waandishi wa Habari za Michezo nchini 'Taswa FC' katika kufanikisha inafanya vizuri katika mashindano mbalimbali ikiwamo yale ya Media Bonanza yanayofanyika kila mwaka mkoani Arusha.Chanzo:fullshangweblog

Monday, June 4, 2012

IKULU:Taswira Za Rais Jakaya Kikwete Akiwa Katika Mazoezi yake ya Kutembea kilomita Tatu kila Asubuhi na Jioni Kabla ya Kufanya Mazoezi ya Viungo na kuingia Gym Katika Kuuweka Mwili Wake Katika Hali ya Ukakamavu na Afya.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete, aliye katika mapumziko mafupi jijini Arusha, akiwa katika mazoezi yake ya kutembea kilomita tatu kila asubuhi na jioni kabla ya kufanya mazoezi ya viungo na kuingia gym, katika kuuweka mwili wake katika hali ya ukakamavu na afya. Wakaazi wengi wa Arusha ambao wamemuona akitembea wamesisimkwa na kufurahishwa sana na hatua hiyo ya kiongozi mkuu wa nchi kuwa mstari wa mbele katika kujenga afya kwa mazoezi ya kila siku, na kutaka kila mtu, si viongozi tu, kuiga mfano wake.Picha na IKULU

Waraka Wa Mheshimiwa Godbless Lema Kwa Rais Jakaya Kikwete

 Aliyekua Mbunge wa Arusha Mjini(CHADEMA)Mheshimiwa Godbless Lema
---

Ndugu Wananchi;

Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa ndugu zetu wa Arusha kwa kuwapokea vizuri na kuwakarimu vyema wageni wetu hao. Nawaomba waendelee na moyo huo mpaka watakapoondoka wote. Naomba kuwepo kwa mkutano huu kuwakumbushe umuhimu wa mji wenu kuwa tulivu. Miaka miwili iliyopita isingekuwa rahisi kwa watu au shirika kubwa la kimataifa kama Benki hii kuamua kufanya mkutano wake Arusha. Isitoshe hata sisi wenyewe tusingeshawishika kuomba au kukubali maombi ya namna hiyo. Lakini sasa imewezekana. Naomba kila mmoja wetu aweke azimio moyoni mwake la kuhakikisha kuwa hali ile haijirudii tena. Nyota ya Geneva ya Afrika lazima iendelee kuangaza. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo . ( J.K . KIKWETE.)

“Narudia tena , IKULU iliingilia kesi yangu ya Ubunge”.

Mh Rais nimekusikiliza kwa makini sana ila nakupa pole kwani bado unafikiri unaongea na Tanzania ya mwaka 1961 , umesema sasa Arusha ni shwari tofauti na miaka miwili iliyopita kwani sasa kuna amani na utulivu wa kutosha ndio maana hata mkutano wa AFDB umefanyika Arusha .

Mh Rais , najua IKULU iliingilia kesi yangu kama ilivyoonekana na ndio sababu hata Mkuu wa Mkoa wa Arusha wakati anaapisha Wakuu wa Wilaya alimpongeza Jaji kwa hukumu nzuri aliyowafurahisha wakati kesi hiyo iko mahakama ya Rufaa , lakini jambo moja la msingi ambalo huwezi kulitambua kwa sasa ni kuwa Haki na Ukweli haviwezi kushindwa na dhuluma, ubaya wala mamlaka , natambua wewe ni Rais na unayo mamalaka makubwa katika Taifa hili lakini vile vile nataka utambue kuwa huna mamlaka makubwa dhidi ya haki , utu na ukweli.

Mh Rais hakuna Amani Duniani inayozidi Haki na usawa ,utu na ukweli , haipo na wala haitakuwepo , ndio maana kila siku nasema ni “Afadhali Vita Inayotafuta Haki na usawa kuliko Amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa Mwanadamu “ umefurahia sana mkutano uliokupa fursa ya kutoa maneno ya kebehi na kudhihirisha ila chafu iliyofanywa na Serikali yako na kujaribu kuhadaa Umma kama ilivyo kawaida ya Serikali yako na Chama chako , hata hivyo wakati huu kuna mambo ya msingi yakushughulikia zaidi ya kebehi na hadaa , Uchumi wa Nchi umeyumba, huduma za msingi za jamii zimepuuzwa, Mpasuko katika suala la Muungano na vururugu zinazoendelea Zanzibar , mfumuko wa bei hizi ni sababu chache ambazo haziwezi kuruhusu wakati huu kuwa wakati wa kebehi na mizaha isipokuwa kazi .

Mh Rais , Mama Theresa , Nelson Mandela , Martin Luther Jr na Malcom X hawakuwa Wabunge kupigania haki za Nchi yao na watu wao , sihitaji Ubunge kupigania ukweli, haki na utu , nahitaji dhamira safi , nia njema na huu utakuwa wajibu wangu mpaka nakwenda kaburini , nitakapomaliza mbio hizi najua nitapata fursa ya kutazama nyuma yangu nione nini nilifanya , ukweli nisingependa kuona vituo vya mafuta , magorofa , magari na viwanja vingi kila kona ya Nchi bali Haki ,Usawa na utu vikiwa kama nguzo ya imani ya watawala wetu watakaokuwepo, pengine sitaishi miaka mingi sana kama utachukizwa sana na waraka wangu huu kwani Polisi , Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi wanakutii wewe , hata hivyo siogopi kufa kwani nisipokufa kesho , nitakufa siku moja ambayo siijui , napenda kuishi maisha marefu nimwone mke wa mtoto wangu kama itawezekana , lakini kuliko iwezekane kwa kuishi kwa hofu ni bora ishindakane kwa kuthamini haki , kwa hiyo kama utakuwa umekasirika sana , unaweza kufanya jambo lolote baya kwa kutumia mamlaka yako , niko tiyari sio kesho wala leo isipokuwa sasa hivi, najua IKULU imewazulumu watu wa Arusha Mbunge wao.

Mh Rais ninajua wazi njama zote na hasira hizi zinaweza kuwa zimetokana hasa na mkutano tuliokaa Osterbay Dar mimi na wewe kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hata hivyo sikupuuza maongezi yetu isipokuwa nilichagua kufuata dhamira yangu na wito wangu wa utumishi wa kweli katika Jimbo langu na Nchi yangu.

Mh Rais nimekuelewa na Wananchi wamekuelewa kila mahali , wewe ni Rais unayo mamlaka makubwa na mimi ni mwananchi mamlaka yangu makubwa ni kwa mke wangu tu , sina Polisi wala Usalama wa Taifa lakini nitawaomba wanyonge wafunge na kusali tuone kama mamlaka yako inaweza kushindana na haki na ukweli .

Mh Rais “Mtu anaweza kuzini kwa siri lakini hawezi kuugua ukimwi kwa siri” Serikali na Chama cha Mapinduzi kimepuuza watu na haki zao kwa muda mrefu , lakini wakati umefika ambapo hawatapuuzwa tena hata hivyo kwa kauli yako hii naamnini haiwezi kuwafundisha kazi majaji wa mahakama ya rufaa .

ONLY TIME WILL TELL”.

GODBLESS .J. LEMA.

MAKAMU WA RAIS DK GHARIB BILAL AZINDUA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI-KILIMANJARO

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwahutubia wananchi wa Mkoani Kilimanjaro, wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani,jana Juni 03, 2012, ambayo yanafanyika Kitaifa Mkoani Kilimanjaro.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akikata utepe kuzindua rasmi maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani,jana Juni 03. 2012, yanayofanyika Kitaifa Mkoani Kilimanjaro.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipanda mti aina ya Mroliondo katika eneo la Chem chem ya Maji Njoro,jana Juni 03, 2012, ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika Kitaifa Mkoani Kilimanjaro.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiangalia mche wa zao la Kahawa wakati akitembelea katika mabanda ya maonyesho alipokuwa akizindua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayoendelea katika Viwanja vya Mashujaa Mkoani Kilimanjaro.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Ofisa Masoko wa Kundi la Mradi wa i WASH, Kelvin Mwanshilo, wa Shirika la Care, kuhusu vyoo mbadala vya Gharama nafuu, wakati alipotembelea katika Banda la kikundi hicho katika maonyesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, yaliyozinduliwa Kitaifa na Makamu wa Rais,jana Juni 03, 2012, Viwanja vya  Mashujaa Mkoani Kilimanjaro.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kikundi cha BEP-Environmental Initiatives Consortium, Jensen Siria, kuhusu matumizi na utengezaji wa majiko ya gharama nafuu, wakati alipotembelea katika Banda la kikundi hicho katika maonyesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, yaliyozinduliwa Kitaifa na Makamu wa Rais,jana Juni 03, 2012, Viwanja vya  Mashujaa Mkoani Kilimanjaro.
Kikundi cha ngoma za asili cha mkoani Kilimanjaro kikitoa burudani.Picha na Muhidin Sufiani-Ofisi ya Makamu wa Rais

Sunday, June 3, 2012

JK Akutana Na Rais Wa Somalia



Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Rais Sheikh Shariff Ahmed aliyekutana naye jana june 2, 2012 jijini Arusha.
Pamoja na mambo mengine Rais Kikwete na mgeni wake waliongelea hali ya usalama katika nchi hiyo ya pembe ya 
Afrika na pia akamhakikishia Rais huyo ushirikiano wa kila aina katika kuhakikisha utulivu unarejea nchini Somalia.

PICHA NA IKULU

Kalou Na Drogba Wainyonga Taifa Stars ( Mwananchi)

 Send to a friend
*Kocha asema makosa yamewagharimu
Edo Kumwembe, Ivory Coast

TANZANIA imeanza vibaya kampeni zake za kucheza Fainali za Kombe la Dunia Brazil 2014 baada ya kufungwa mabao 2-0 na Ivory Coast.

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny, Stars ilijitahidi kucheza kandanda la kawaida kwa pasi za kawaida tofauti na ilivyotarajiwa.

Ikiwa ni mtihani wa pili kwa kocha wake, Kim Poulsen baada ya mchezo wa kwanza wa kirafiki na Malawi kutoka 0-0, Stars ilipoteana dakika ya tisa tu na kufungwa bao kirahisi lililowekwa kimiani na Solomon Kalou.

Kalou aliwapiga chenga mabeki watatu wa Stars baada ya kuunasa mpira mguuni kwa Kelvin Yondan aliyezubaa kuuondosha akiwa ndani ya eneo la hatari.

Baada ya bao hilo, Stars ilijipanga upya na kuelekeza mashambulizi langoni kwa wapinzani wao na dakika ya 14, Aggrey Moris alipiga mpira wa adhabu uliogonga mwamba lakini hata hivyo, wachezaji wa Ivory Coast walikuwa makini kuondosha.

Katika dakika ya 22, Didier Drogba naye aligongesha mwamba kwa mpira wa adhabu iliyosababishwa na Morris baada ya kumkwatua Kalou akiwa nje kidogo ya eneo la hatari. Morris alionyeshwa kadi ya njano kwa faulo hiyo.

Dakika mbili baadaye, ushirikiano wa Mbwana Samatta na Morris aliyepanda kusaidia mashambulizi nusura uzae bao lakini hawakuwa makini.

Beki huyo anayechezea Azam alipiga kombora lililotokana na mpira wa adhabu baada ya Mwinyi Kazimoto kukwatuliwa ndani ya eneo la hatari na Tiote lakini hata hivyo likatoka nje.

Stars iliendelea kuliandama lango la wapinzani wao na katika dakika ya 36, ilipata kona tatu mfululizo zilipigwa na Amir Maftah lakini hata hivyo zilikuwa tasa. Dakika ya 40 hadi kumalizika kipindi cha kwanza, Stars ilicheza pasi za hapa na pale na kuwachanganya Ivory Coast.

Kipindi cha pili kilianza taratibu na hata hivyo Stars iliyokuwa na uchu nusura ipate bao dakika ya 62 lakini kichwa cha Samatta hakikulenga lango, kabla ya Gervinho kujibu dakika mbili baadaye baada ya kumtoka Maftah.

Kocha wa Ivory Coast, Sabri Lamouchi alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Gervinho na Tiote na nafasi zao kuchukuliwa na Kader Keita na Konnan Didier.

Stars ilipata pigo dakika ya 63 baada ya beki wake wa kati, Morris kulimwa kadi nyekundu kwa kumkwatua Kalou ikiwa ni kadi ya pili ya njano. Kuona hivyo, Kim Poulsen alimtoa Salum Aboubakar na nafasi yake kuchukuliwa na John Boko.

Dakika ya 70, Didier Drogba aliipatia Ivory Coast bao la pili kwa mpira wa kichwa baada ya kuunganisha krosi ya Keita. Kuona hivyo, Poulsen alimtoa Boko na kumuingiza Erasto Nyoni kwa ajili ya kuimarisha safu ya ulinzi.

Lolo Alexander alimchezea rafu mbaya Kazimoto na hakuweza kurudi uwanjani katika dakika ya 89. Stars ilishindwa kufanya mabadiliko kutokana na kumaliza wachezaji wake wote wa akiba

Katika mchezo huo Stars iliwakilishwa na: Kaseja, Kapombe, Maftah, Yondan, Agrey Morris, Shaaban Nditi, Salum Aboubakar/John Boko, Frank Domayo, Mbwana Samatta, Ngassa na Mwinyi Kazimoto.

Ivory Coast: Bary Boubacar, Emmanuel Eboue, Tiene Siaka, Kolo Toure, Lolo Igor, Gosso Gosso Jean, Yao Kouassi, Cheikh Tiote, Didier Drogba na Solomon Kalou.Chanzo: Mwananchi

Tamko La Wakristo Kuhusu Machafuko Na Vitisho Zanzibar


Kanisa Katoliki la mpendae lililochomwa moto hivi karibuni Zanzibar



Sisi Maaskofu, Mapadre, Wachungaji na Waumini tunaoishi Zanzibar, tumekutana leo tarehe 30
Mei 2012 kufuatia hali ya machafuko, uvunjifu wa amani, uchomaji wa Makanisa, uharibifu wa
mali za Kanisa na vitisho dhidi ya Wakristo na mali zao.

Tumekutana na tunatoa tamko baada ya muda mrefu wa kimya na uvumilivu tuliosafiri nao kwa
takaribani miaka 11, kwa kumbukumbu zetu tangu mwaka 2001. Tunajua na tunauambia umma
wa wapenda amani kuwa matukio ya tarehe 26 hadi 28 Mei 2012 ni matokeo ya mahubiri na
mihadhara ambayo imekuwa ikiendeshwa iliyolenga kwa makusudi kuutukana na kuukashifu
Ukristo hapa visiwani Zanzibar na hivi kupandikiza hofu miongoni mwa waumini wa dini ya
Kikristo. Tunashawishika kusema kuwa ufadhili na ushawishi wa vurugu na vitisho hivi vina
udhamini wa ndani au nje ya nchi yetu.

Tumefikia hatua hiyo baada ya matukio mbalimbali yaliyokuwa yanafanywa dhidi ya Kanisa
na mali zake tangu mwaka wa 2001 hadi ya hivi majuzi yalikuwa yakitolewa taarifa kwenye
vyombo vya Ulinzi na Usalama hapa Visiwani Zanzibar; lakini ushirikiano umekuwa mdogo,
na kwa sehemu kubwa dhaifu sana. Kwa malezo na vielelezo ni kwamba, jumla ya makanisa
yasiyopungua 25 yamevunjwa na kuchomwa moto tangu mwaka 2001, pamoja na ahadi za
Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo yote yaliyopata kutolewa taarifa
hakuna hata moja lililothibitika wahusika kukamatwa, kufikishwa mahakamani na kuchukuliwa
hatua za kisheria. Kumekuwa pia na vitendo vya kuchoma magari huko Pemba na hapa
Unguja, na Serikali kwa upande wake imeshiriki hata kupora ardhi na majengo ya Kanisa hapa
Unguja na huko Pemba .

Tumebaini pia hasa baada ya matukio ya vurugu za tarehe 26 hadi 28 Mei 2012 kuwa kuna
mikakati ya makusudi ya kuwafanyia Wakristo vurugu. Mikakati hiyo inajumuisha mambo
kama vile kuchoma Makanisa zaidi, kuharibu mali za Makanisa yakiwemo mashule, na vituo
mbalimbali vya Kanisa vinavyotoa huduma za kijamii hapa Visiwani.

Mkakati au mpango huo umepangwa na unakusudiwa kutekelezwa kati ya tarehe 1 na 2 Juni,
na tarehe 8 na 9 Juni mwaka huu. Tunazo taarifa tunazoweza kuzithibitisha kuwa baadhi ya
Wakristo wamekuwa wakitumiwa jumbe za simu za mkononi (SMS) zikiwatisha na kuwataka
waondoke visiwani humu mara moja hata kama ni wazawa.

Sehemu ya pili ya mkakati ni kuwasaka Wakristo nyumba kwa nyumba kwaajili ya
kuwaangamiza, kuwabaka na kuwalawiti.

Chakusikitisha zaidi ni pale ambapo baadhi ya walinzi wa Usalama wa raia hasa Polisi wenye
asili ya hapa Visiwani Zanzibar kusikika wakisema kuwa wataunga mkono vurugu kila
zitakapotokea.

Kufuatia maelezo hayo yote, Sisi Maaskofu, Wachungaji, Mapadri na Waumini tuliokutana
leo, tunapenda kwanza kutoa neno la shukrani kwa uongozi wa Serikali yetu kwa ushirikiano
iliyouonyesha kufuatia matukio ya hivi majuzi, na hasa kwa kupewa fursa za kukutana na

viongozi na kusikilizwa.

Tunatamka kuuelezea umma wa wapenda Amani wote tukisema, tumechoshwa kuishi na
kuchukuliwa kama raia wa daraja la pili katika nchi yetu. Tunaonya kuwa hatuko tayari tena
kuvumilia vitendo vya uvunjaji wa amani na haki zetu na tabia za kufanywa tuishi kwa hofu.

Kadhalika tunaiomba serikali yetu ituhakikishie usalama wa maisha yetu, mali zetu pamoja na
majengo yetu ya Ibada.

Wito wetu kwa viongozi wa dini mbalimbali hapa nchini ni kuwa, kila mmoja anawajibu mkubwa
wa kuhakikisha kwamba nchi yetu inatawaliwa kwa mujibu wa sheria za nchi na kwamba kila
mmoja ahubiri kwa lengo la kukuza amani, utulivu na usalama wa kila mtu na mali zake.

Mwisho, tunapenda kuhitimisha tamko letu kwa kuwaalika wakristo wote kuiombea nchi yetu
amani, utulivu na mshikamano ambazo ni tunu tulizoachiwa na waasisi wetu.

Ni imani yetu pia kwamba viongozi wetu watatekeleza wajibu wao na mamlaka waliyopewa na
Mungu pasipo upendeleo wa aina yoyote.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Zanzibar.

Kwa niaba ya Wakristo wote;

Ni sisi Maaskofu wenu

………………………………………………………

1. Michael Hafidh
Askofu wa Kanisa Anglikana Zanzibar

……………………………………………
2. Augustine Shao
Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar

……………………………………………
3. Pastor Timothy W. Philemon
Makamu Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji wa Makanisa ya Pentekoste
Zanzibar

Saturday, June 2, 2012

IKULU:Rais Jakaya Kikwete Akutana na Mmiliki wa Klabu ya Portsmouth Ikulu Jijini Dar Es Salaam

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Royal Group ya Saudi Arabia, Dkt. Sulaiman Al Fahim wakati walipokutana leo, Jumamosi, Juni 2, 2012, Ikulu Dar es Salaam. Dkt. Al Fahim ambaye ni mwenyekiti wa zamani na mmilikimwenza wa Klabu ya soka ya Portsmouth ya Uingereza yuko nchini kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika uchumi wa Tanzania. Dkt. Al Fahim pia ndiye aliyeongoza mazungumzo na kununuliwa kwa klabu bingwa ya Ligi Kuu ya Uingereza ya Manchester City na Kampuni ya Arabuni.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na  Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Royal Group ya Saudi Arabia, Dkt. Sulaiman Al Fahim wakati walipokutana leo, Jumamosi, Juni 2, 2012, Ikulu Dar es Salaam. Dkt. Al Fahim ambaye ni mwenyekiti wa zamani na mmilikimwenza wa Klabu ya soka ya Portsmouth ya Uingereza yuko nchini kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika uchumi wa Tanzania. Dkt. Al Fahim pia ndiye aliyeongoza mazungumzo na kununuliwa kwa klabu bingwa ya Ligi Kuu ya Uingereza ya Manchester City na Kampuni ya Arabuni.Picha na Fredy Maro-IKULU

JESHI LA POLISI MKOANI KIGOMA WAOKOA WATATU WANAOTUHUMIWA KWA UCHUWI

 BAADHI YA WANANCHI WAKISHANGAA BAADA YA FAINES KUZINDULIWA NA MTOTO MWENYE MIAKA KUMI ALIYEKABIDHIWA MIKOBA NA MAMA YAKE.
 BIBI NA MJUKUU WAKE WANAOSADIKIWA NI WACHAWI WAKIWA KATIKA GARI LA POLISI.
 FAINES AKIPAKIWA KATIKA GARI YA POLISI.
FAINES ZAWADI-BINTI ALIYEFARIKI KWA MUDA NA KUREJESHWA DUNIANI AKIWA AMESHIKILIWA NA NDUGU ZAKE.
---
 
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limefanikiwa kuwaokoa watu watatu waliokuwa wamezingirwa na kundi la wananchi wakitaka kuwaua kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ushirikina.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma SSP Joseph Konyo, aliwataja watu hao waliokolewa kuwa ni Evania Sephanga(50), mkazi wa wilaya ya Kibondo, Bruno January(46), mkazi wa kijiji cha Nyamhoza na mtoto mmoja mwenye umri wa miaka kumi na mkazi wa kijiji cha Nyamhoza Kigoma mjini ambaye jina lake linahifadhiwa.
 
 
Kamanda Konyo amesema kuwa wiki iliyopita majira ya saa tisa mchana, watu hao walizingirwa na kundi hilo kwa madai kuwa walimroga na kumuua msichana mmoja aitwaye Faines Zawadi(20) mkazi wa kijiji hicho cha Nyamhoza ambaye siku moja kabla ya kifo chake alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa na kuwa kama kichaa.

Alisema katika tukio hilo, bibi kizee mmoja ambaye alikuwa mshirika wa kundi la waliodaiwa kuwa wachawi, alifanikiwa kutoroka katika mazingira ya kutatanisha alipojifanya kuwa anakwenda kujisaidia.
 
 
Kamanda Konyo amemtaja bibi huyo aliyefanikiwa kutoroka kuwa ni Bibi Editha Dosiyo mkazi wa kijiji hicho ambaye baadaye alipatikana na kuhojiwa kabla ya kukabidhiwa kwa Idara ya ustawi wa jamii baada ya kuonekana kuwa maisha yake yangekuwa hatarini.

Amesema baada ya Polisi kupata taarifa za tukio hilo, walikimbia na kwenda kuwaokoa kutoka katika mikono ya kundi la wananchi lakini wakiwa wameshaadhibu ingawa ilikuwa haijawa kwa kiasi kikubwa.

Habari zinasema kuwa, baadhi ya wananchi walipata taarifa kutoka kwa mtoto aliyeokolewa akisema kuwa baadhi ya watoto waliofariki kijijini hapo, akiwataja (majina tunayahifadhi) alikuwa akiwaona nyumbani kwao nyakati za usiku wakiosha vyombo na baadaye kupewa chakula.

Siku ya tukio hilo, baadhi ya wananchi walisema kuwa kabla ya bibi huyo kutoweka alimnong’oneza jambo mjukuu wake ili amfanyie mareheme ikiwa ni pamoja na kumruka mara saba kisha bibi huyo alitoweka akijifanya anakwenda kujisaidia.
 
 
Walisema mara baada ya bibi huyo kutoweka, mtoto huyo wa kiume ambaye ni miongoni mwa waliozingirwa wakitaka kuuawa, aliamza kutekeleza maagizo ya bibi huyo na alipomaliza kitendo cha kumruka kwa mara ya saba, msichana yuyo ambaye alikuwa ni marehemu alizinduka na kuomba uji.

Wamesema msichana huyo ambaye alikuwa mfu, alipewa uji na kunywa kisha akapelekwa hospitalini ambako hadi sasa hali yake inasemekana kuwa inaendelea vizuri.

Hata hivyo Kamanda Konyo ametoa wito kwa wananchi kuacha kuchukua sheria mkononi na badala yake watoe taarifa Polisi kwa kila jambo wanaloliona kuwa linaweza kuleta uvunjifu wa amani ili hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Mwezi uliopita watu wawili mke na mume, waliuawa na kundi la watu wenye hasira kisha miili yao kuchomwa kwa moto mkoani Kigoma baada wa kutuhumiwa kuwa walikuwa ni wachawi.

Na 
Pardon Mbwate na Felister Chubwa,
 Polisi -Kigoma

Friday, June 1, 2012

MIZENGO PINDA AMWAKILIHA RAIS JAKAYA KIKWETE KIKAO CHA SADC

 

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikaribishwa kwa gwaride baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Luanda, Angola May 31, 2012 kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika Kikao cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC. Anaongozwa na Waziri wa  Nishati na Maji wa Angola  Joao Baptista Borges. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikaribishwa kwa gwaride baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Luanda, Angola May 31, 2012 kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika Kikao cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC. Anaongozwa na Waziri wa  Nishati na Maji wa Angola  Joao Baptista Borges. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza  na Waziri wa Nishati na Maji wa Angola, Joao  Baptista Borges baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Luanda nchini Angola May  31, 2012 ambako atamwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika kikao cha  Wakuu wa Nchi za  Jumuiya  ya Maendeleo  ya Kusini mwa Afrika SADC Juni 1, 2012. (Picha na Ofisi  ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe baada ya kuwasili Luanda Angola May 31, 20121 ambako atamwakilisha Rais Jakaya Kikwenye katika Kikao cha Wakuu wa Nchi  za Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika SADC Juni 1, 2012. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengio Pinda akisalimiana na Rais wa Angola Jose Edwardo dos  Santos katika kikao cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleoo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC kilichofanyika  Juni 1, 2012 Mjini Luanda Angola . (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Rais Dk. Shein akutana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais,Mikoa


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Uongozi wa Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mikoa ikiwa ni utaratibu wake wa
kuzungumza na kila wizara katika utekelezaji wa kazi katika Mikoa.
[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Uongozi wa Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mikoa ikiwa ni utaratibu wake wa
kuzungumza na kila wizara katika utekelezaji wa kazi katika
Mikoa,(kushoto) Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif Hamadi.
[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]